News & Events

dawasa_small

TAARIFA YA MRADI WA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAJISAFI NA MAJITAKA KATIKA MJI WA BAGAMOYO YA VITONGOJI VYAKE
AGOSTI 2016.

A. UTANGULIZI

     Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA) inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kuboresha huduma kwa wakazi waishio katika eneo lake la huduma ambalo ni jiji la Dar es salaam, Kibaha na Bagamoyo na maeneo yaliyo kando ya mabomba makuu kutoka Mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini.

 Miradi hiyo ni pamoja na upanuzi wa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, uchimbaji wa visima vya uchunguzi kuzunguka mwamba wa Kimbiji, Uchimbaji wa visima vya uzalishaji Kimbiji na Mpera, ujenzi wa bwawa la Kidunda, Upanuzi wa mfumo wa usambazaji majisafi na ujenzi wa mfumo wa ukusanyaji na kutibu majitaka.

Lengo la miradi ya uzalishaji majisafi ni kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 502 za sasa na kufikia lita milioni 756 ifikapo mwakani. Kiasi cha maji yanayohitajika kutosheleza mahitaji ya wakazi walio katika eneo la huduma la DAWASA ni lita milioni 450 hivyo, maji yanayozalishwa yanatosha mahitaji kwa sasa, kazi iliyobaki ni kuyasambaza kwa wananchi.

   Aidha mradi wa upanuzi wa mfumo wa usambazaji maji unalenga katika kuwezesha maji yatakayozalishwa kuwafikia wananchi katika maeneo yasiyo na mfumo rasmi wa usambazaji maji na hivyo kupanua wigo wa utoaji wa huduma. Awamu hii itahusisha maeneo ya Mbezi hadi Kiluvya na Tegeta hadi Bagamoyo.

B. MIRADI KATIKA WILAYA YA BAGAMOYO

          DAWASA inatekeleza miradi mikubwa mitano katika Wilaya ya Bagamoyo inayohusu kuboresha huduma ya majisafi na majitaka. Miradi inayotekelezwa ni:-

1. Upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Chini; – Ulioongeza uzalishaji kutoka lita milioni 180 hadi 270 kwa siku

        Mradi huu ulihusisha upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo ili kuongeza uzalishaji kutoka lita milioni 180 kwa siku kufikia lita milioni 270 kwa siku. Mradi huu umekamilika na mtambo unafanya kazi kama ulivyokusudiwa. Maeneo mengi hivi sasa yanapata maji ya kutosha, changamoto iliyopo kwa sasa ni kuongeza mtandao wa mabomba ya usambazaji; kazi ambayo inashughulikiwa kupitia miradi mipya ya usambazaji maji iliyoanza.

2. Mradi wa Bomba Kuu Kutoka Mtambo wa maji wa Ruvu Chini kwenda DSM kupitia BAGAMOYO (Lower Ruvu Transmission Pipeline)

        Mradi huu ulihusu ujenzi wa bomba kubwa lenye kipenyo cha mm 1800 na umbali wa km 55 ili kusafirisha maji kutoka mtamboni kwenda DSM kupitia Bagamoyo. Mradi huu umekamilika na tayari bomba jipya linatumika sambamba na lile la zamani.

3. Mradi wa Ujenzi Matenki Makubwa na Mabomba ya Kusafirisha maji na kusambaza kwa wateja (Package 2F na Delegated Work Part 2) kuanzia Mpiji hadi Bagamoyo Mjini na Vitongoji vyake

       Mradi huu unajumuisha kazi za ujenzi wa matenki makubwa mawili ya kuhifadhi maji yatajengwa Bagamoyo mjini na Eneo la uwekezaji la Bagamoyo, mabomba makubwa ya kusogeza maji kutoka bomba kubwa la Ruvu Chini kwenda kwenye matenki ya kuhifadhi maji, mabomba ya kusafirisha maji km 3.8 yenye ukubwa wa mm 250 na 300, mabomba ya kusogeza maji kwa wananchi km 26.4 yenye ukubwa wa mm75 hadi 200mm, mabomba madogo madogo ya kuunganisha wateja na kuunganisha wateja 35,000.

      Pamoja na mji wa Bagamoyo, maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huu ni Mpiji, Mapinga, Zinga, Kiromo, Kitopeni, Ukuni, Kerege, Buma, Mataya, Magereza, Miswe, Mbwawa, Chasimba, Kongo na maeneo yote ya jirani. Katika maeneo haya, mradi utajenga mabomba ya kusafirisha maji km 8.6 yenye ukubwa wa mm 250 na 300, na km 62 yenye ukubwa wa 75mm hadi 200mm, mabomba ya kusogeza maji kwa wananchi km 22.7 yenye ukubwa wa mm110 hadi 300mm, mabomba madogo madogo ya kuunganisha wateja 35,000, ujenzi wa matenki 7 yenye ujazo kati ya lita laki 2 hadi milioni 1, viosk 42 na kuunganisha wateja 35,000.

4. Mradi wa Upanuzi wa Chanzo cha maji Wami na mabomba ya kusambaza maji kwa wananchi (Chalinze Phase III)

           Mradi huu unalenga kuongeza uzalishaji maji katika mtambo wa maji Wami kutoka mita za ujazo 500 kwa saa hadi lita 900 kwa saa, ujenzi wa mabomba ya kusafirisha maji na kusambaza maji kwa wananchi yenye urefu wa kilomita zisizopungua 1048, Matenki makubwa 19 kwa ajili ya kuhifadhi maji yenye, Vituo 9 vya kusukuma maji (Booster stations) na Vioski (vituo) vya kuchotea maji 499.

            Mradi huu unanufaisha Zaidi wakazi wa wilaya ya Bagamoyo wanaotumia maji kutoka mtambo wa Wami. Maeneo hayo ni pamoja na vijiji 67 (ambapo vijiji 18 viko kaskazi mwa mto Wami na 49 Kusini mwa Wami. Baadhi ya vijiji ni Msata, Masuguru, Mwetemo, bago, Kiwangwa, Mwavi, Fukayosi, Makurunge na Kidomole.

5. Mradi wa Ujenzi wa Mfumo wa Kukusanya na Kutibu Majitaka (Bagamoyo Sewerage Project)

         Katika azma ya Serikali kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira, DAWASA itatekeleza mradi wa kukusanya majitaka na kuyasafisha. Awamu ya kwanza itahusu eneo la mji wa Bagamoyo na eneo la uwekezaji la Bagamoyo SEZ. Awamu zitakazofauata zitahusu maeneo mapya yaliyo nje ya mji. Kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa Mitambo ya Kuchuja na kusafisha Majitaka, Mabomba ya kukusanya na vituo vya kusukumia majitaka.

C. FAIDA ZA MIRADI INAYOTEKELEZWA

Miradi ikikamilika itaboresha huduma ya majisafi na majitaka hivyo kuboresha afya za wakazi, kuongeza kipato kwa kufanya shughuli halai zinazohitaji maji, akina mama watapata muda wa kufanya shughuli za maendeleo na kujiongezea kipata.

• Huduma ya majisafi zitapatikana katika eneo la Makazi na eneo Maalum la Uchumi Bagamoyo mwaka mzima pamoja

• Mradi wa majitaka utawezesha uondoshaji majitaka katika maeneo ya viwanda na makazi utapunguza uchafuzi wa mazingira na kupunguza magonjwa ya milipuko kama vile Kuhara na Kipindupindu

• Mradi utasaidia kuvutia wawekezaji kwa kuwapatia huduma bila wao kuhitajika kuwekeza katika kujiletea huduma hizi wao wenyewe,

• Mradi utasaidia kuhakikisha kuwa huduma za ujenzi wa mji mpya zinakamilka kwa wakati baada ya huduma ya maji kufika eneo hilo,

• Mradi utasaidia utunzaji wa mazingira kwa kuhudumia kusafisha majitaka,

• Mradi pia utachangia pato la Taifa kwa kusaidia shughuli za uzalishaji katika viwanda

D. CHANGAMOTO KATIKA UTEKELEZAJI MIRADI

• Gharama kubwa ya miradi ya ujenzi
• Uhaba wa maji kulinganisha na mahitajIi
• Ujenzi wa makazi usiozingatia taratibu za mipango miji
• Ukame, Uvamizi na uchafuzi wa vyanzo vya maji.
• Uvamizi wa hifadhi ya miundombinu ya maji
• Uhaba wa maeneo ya kujenga miundombinu ya maji
• Kesi zilizofunguliwa kuzuia ulazaji wa mabomba makuu

       Changamoto hizi zinapunguza kasi ya utekelezaji wa miradi hata hivyo, mamlaka kwa kushirikaina na taasisi zingine za Serikali zinakabiliana na changamoto hizi na kumekuwa na maendeleo ya kuridhisha

E. HATUA YA UTEKELEZAJI

Hadi kufikia Agosti 2016 utekelezaji wa miradi hii ulikuwa kama ifuatavyo:

Mradi Hatua iliyofikiwa Gharama
1. Upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Chini kutoka uzalishaji wa lita milioni 180 hadi 270 kwa siku Kazi imekamilika USD Milioni 36.8 sawa na shilingi bilioni 80.96
2. Ulazaji wa bomba kuu kutoka Ruvu Chini lenye kipenyo cha mita 1.8 umbali wa km 56 Kazi itakamilika Shilingi bilioni 141.5
3. Mradi wa Matenki Makubwa na Mabomba ya Kusafirisha maji na kusambaza kwa wateja (Package 2F na Delegeted Works Part 2)
Ujenzi umeanza Machi 2016 na utakamilika Juni 2017. US$ milioni 32 sawa na shilingi billion 70.4 (Mkataba umechanganya kazi za DSM na Bagamoyo,)
4. Mradi wa Upanuzi wa Chanzo cha maji Wami na mabomba ya kusambaza maji kwa wananchi (Chalinze Phase III)
Ujenzi ulianza Novemba 2015 na utakamilika Februari 2017 US$ milioni 41 sawa shilingi bilioni 90.2.
5. Mradi wa Ujenzi wa Mfumo wa Kukusanya na Kutibu Majitaka (Bagamoyo Sewerage Project)
Kazi ya usanifu wa mradi imeanza Agosti 2016 na itakamilika Desemba 2016. Ujenzi utaanza baada ya kupata fedha za ujenzi Usanifu US$ 366,655 sawa na shilingi milioni 806.41

F. HITIMISHO

       DAWASA inaona fahari kushiriki na wananchi wa Mji wa Bagamoyo katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais la kufanya usafi katika maeneo mbali mbali ya nchi. Bagamoyo iko ndani ya eneo tunalolihudumia na kwa sasa tutaonekana sana kwani kazi zetu za ujenzi wa miradi zinahitaji ushirikishwaji wa jamii ili kuhakikisha huduma yetu inakuwa nafuu na endelevu.

    Katika utekelezaji wa miradi inayoendelea DAWASA itahitaji maeneo ya kujenga miundombini kama vile Matenki ya maji, viosk vya kuchota maji na kulaza mabomba. Tunaomba uongozi wa Wilzya na Wananchi kwa ujumla kutusaidia.

      Tunatoa shukurani za dhati kwa uongozi wa Wilaya kuturuhusu kushirikiana na wananchi katika zoezi hili la leo na tutaendelea kushirikiana ili kuleta maendeleo ya haraka Bagamoyo na katika eneo zima linalohudumiwa na DAWASA.

HAPA KAZI TU.
MAJI NI UHAI
USAFI WA MAZINGIRA NI UTU

ASANTENI.
______________________________
IMETOLEWA NA AFISA MTENDAJI MKUU
DAWASA, 27/08/2016

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikishirikiana na Serikali ya India, katika kuchangia maendeleo ya nchi katika nyanja mbalimbali zikiwemo kiuchumi,kielimu na kiutamaduni. Kwa upande waSekta ya maji, miradi mingi imetekelezwa kwa ushirikiano wa nchi mbalimbali ikiwemo Serikali ya India. Hali hii imewezesha kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma ya maji kufika asilimia 86 kwa Miji Mikuu ya Mikoa, asilimia 72 Katika Jiji la Dar es Salaam na asilimia 60 katika Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa.

Soma Zaidi hapa Miradi ya Maji