Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
‎PROF. KABUDI APONGEZA DAWASA UWEKEZAJI MIRADI YA USAFI WA MAZINGIRA
06 Aug, 2026
‎PROF. KABUDI APONGEZA DAWASA UWEKEZAJI MIRADI YA USAFI WA MAZINGIRA

‎Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba John Kabudi, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa hatua zinazochukuliwa katika kuboresha huduma za usafi wa mazingira, hususan sekta ya majitaka.

‎Prof. Kabudi ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kuchakata Majitaka Buguruni wenye thamani ya shilingi Bilioni 190 ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 33.

‎Katika ziara hiyo, Prof. Kabudi alipokea taarifa ya kina kuhusu maendeleo ya mradi huo, hatua zilizofikiwa katika ujenzi, teknolojia inayotumika pamoja na manufaa yanayotarajiwa kupatikana baada ya kukamilika kwake.

‎Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Prof. Kabudi amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha huduma za usafi wa mazingira na kulinda afya za wananchi.

‎“Utekelezaji wa mradi huu ni ishara ya jitihada za Serikali za kuboresha huduma za jamii kwa wananchi. Kukamilika kwake kutaongeza uwezo wa ukusanyaji na uchakataji wa majitaka, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuboresha maisha ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam,” amesema Prof. Kabudi.

‎Ametoa rai kwa wasimamizi na watekelezaji wa mradi kuhakikisha unakamilika kwa wakati, huku wakizingatia ubora wa kazi na usanifu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na mradi unakuwa na tija iliyokusudiwa.

‎Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Miradi DAWASA, Mhandisi Christian Gava, amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Korea, na kwa sasa umefikia asilimia 33 ya utekelezaji, ikiwa ni hatua iliyo mbele ya muda uliopangwa.

‎Amesema kazi zinazoendelea kwa sasa zinahusisha ujenzi wa miundombinu muhimu ya mtambo, ikiwemo majengo ya mitambo, mifumo ya kusafirisha majitaka pamoja na maandalizi ya kufunga vifaa vya kisasa vya uchakataji.

‎“Kazi zinazoendelea kwa sasa zinahusisha ujenzi wa miundombinu muhimu ya mtambo, ikiwemo majengo ya mitambo, mifumo ya kusafirisha majitaka na maandalizi ya kufunga vifaa vya kisasa vya uchakataji,” amesema Mhandisi Gava.

‎Ameeleza kuwa baada ya kukamilika, mradi huo utaongeza uwezo wa kuchakata majitaka kwa ufanisi, kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira na kuboresha huduma za usafi wa mazingira kwa maelfu ya wakazi wa Buguruni na maeneo jirani.

‎Mradi wa Kuchakata Majitaka Buguruni ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu ya usafi wa mazingira jijini Dar es Salaam, kuongeza uwezo wa uchakataji wa majitaka na kupunguza athari zake kwa mazingira na afya za wananchi.