MRADI WA MAJI MBWAWA
TAARIFA YA MRADI WA MAJI MBWAWA
Huduma ya majisafi ni mojawapo ya hitaji muhimu linalochochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja pamoja na kukuza uchumi kwenye ngazi ya taifa.
Majisafi imekuwa hitaji muhimu katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kukuza uchumi hususani za viwandani, mifugo, kilimo, na usafirishaji sambamba na utoaji wa huduma ikiwemo huduma ya afya, elimu na kadhalika.
Kata ya Mbwawa iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani ni mojawapo ya maeneo ambayo yamenufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka kwa kutekeleza miradi ya majisafi.
UTANGULIZI;
Kata hii yenye idadi ya wakazi zaidi ya 6,200, iligundulika kuwa na tatizo la upatikanaji mdogo wa maji kutokana na ongezeko la idadi ya watu walioanzisha makazi na kuzidi uwezo wa mfumo wa usambazaji maji kwenye eneo hilo.
Tangu mwaka 2012, wakazi wa Kata ya Mbwawa iliyopo kilomita 8 kaskazini mwa mji wa Mlandizi kuelekea Wilaya ya Bagamoyo, walikua wakipata huduma ya maji kutoka kwenye mtandao wa tanki la maji la lita laki moja linalopokea maji kwenye mtambo wa Ruvu chini.
Kwa wakati huo, mtandao ulikua unahudumia wakazi wapatao 4,000. Kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi kwenye Kata hiyo, zilichochea ongezeko la watu hali iliyosababisha kuwepo na uhitaji mkubwa wa huduma ya maji.
CHIMBUKO LA MRADI;
Mnamo mwaka 2020 mwezi wa saba, akiwa kwenye mkutano na wananchi Wilaya ya Kibaha, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Mhe. Dkt John Magufuli baada ya kusikia kilio cha wananchi kuhusu shida ya maji, aliiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha wananchi wa Kata hiyo wanapata maji kikamilifu pasipo na usumbufu.
Alisema kuwa wananchi wa Mbwawa wanahaki sawa na wananchi wengine, hivyo huduma ya maji inatakiwa kuwa ya uhakika, nataka DAWASA kushughulikia shida hii ya upatikanaji mdogo wa huduma ya maji kwenye kata hii.
UTEKELEZAJI WA MRADI;
Mradi ulianza kutekelezwa mwezi wa saba mwaka 2020 kwa lengo la kupanua mtandao wa usambazaji maji baada ya mtandao uliokwepo kuzidiwa na idadi ya watu wa Kata hiyo.
Hali hiyo ya uhitaji wa huduma ya maji iliibuka pia kwenye eneo la Miswe lililopo kilomita 6 toka Mbwawa kuelekea Bagamoyo. Baadhi ya maeneo ya Miswe yalikua hayapati maji kwa uhakika kutokana na kuwepo kwa msukumo mdogo wa maji.
Hivyo mwaka 2020, Serikali kupitia DAWASA ilifanya utafiti wa kubaini njia bora ya kutatua upatikanaji mdogo wa maji katika Kata ya Mbwawa na kushauri kusanifiwa kwa mradi wa kutumia chanzo cha maji ya mtambo wa Ruvu chini.
Utekelezaji ulihusisha kazi zifuatazo;
- Ulazaji wa mabomba ya inchi 8 kwa urefu wa kilomita 8.23.
- Ujenzi wa mtandao wa usambazaji maji wa bomba la inchi 6 kwa urefu wa kilomita 7.42.
- Ulazaji wa mabomba ya inchi 4 kwa umbali wa kilomita 4 na 6 kutoka kwenye tanki la maji na kusambaza maji kwa wateja.
- Kazi ya kuhakiki mitambo ya kusukuma maji toka kwenye chanzo kwenda kwenye tanki la maji ili kuwezesha maji kupatikana kwa uhakika.
- Mradi umejenga mtandao wa maji wenye jumla ya kilomita 25.65 kutoka kwenye bomba la inchi 30 lililopo ndani ya mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu hadi kiwanda cha Mbwawa, Kata iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.
HALI YA MRADI;
Mradi umetekelezwa kwa jumla ya bilioni 1.1 ambazo ni fedha za ndani za Mamlaka. Mradi umekamilika na umeshaunganisha wananchi mbalimbali wa Kata hiyo na huduma ya majisafi.
Mradi unauwezo wa kusafirisha kiasi cha lita za ujazo milioni mbili (2,000,000) kwa siku ambazo zinatosheleza mahitaji ya wananchi 6,200 wa Kata ya Mbwawa.
